Bad Advertisement?

News / Reviews:
 • World News
 • Movie Reviews
 • Book Search

  Are you a Christian?

  Online Store:
 • Visit Our eBay Store • SWAHILI BIBLIA - LUKE 21

  JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


  21:1 Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu,

  21:2 akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo.

  21:3 Basi, akasema, "Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote.

  21:4 Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi."

  21:5 Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema,

  21:6 "Haya yote mnayoyaona--zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."

  21:7 Basi, wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?"

  21:8 Yesu akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye`, na, `Wakati ule umekaribia`. Lakini ninyi msiwafuate!

  21:9 Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado."

  21:10 Halafu akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine.

  21:11 Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani.

  21:12 Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu.

  21:13 Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema.

  21:14 Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea,

  21:15 kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga.

  21:16 Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa.

  21:17 Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu.

  21:18 Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.

  21:19 Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.

  21:20 "Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa.

  21:21 Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini.

  21:22 Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie.

  21:23 Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.

  21:24 Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.

  21:25 "Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.

  21:26 Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.

  21:27 Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.

  21:28 Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia."

  21:29 Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti mingine yote.

  21:30 Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

  21:31 Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.

  21:32 Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka.

  21:33 Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita.

  21:34 "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla.

  21:35 Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote.

  21:36 Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu."

  21:37 Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko.

  21:38 Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.

  IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

  God Rules.NET
  Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine