Bad Advertisement?

News / Reviews:
 • World News
 • Movie Reviews
 • Book Search

  Are you a Christian?

  Online Store:
 • Visit Our eBay Store • SWAHILI BIBLIA - LUKE 4

  JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


  4:1 Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.

  4:2 Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.

  4:3 Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate."

  4:4 Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Mtu haishi kwa mkate tu."`

  4:5 Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,

  4:6 "Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.

  4:7 Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu."

  4:8 Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."`

  4:9 Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu,

  4:10 kwa maana imeandikwa: `Atawaamuru malaika wake wakulinde,`

  4:11 na tena, `Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."`

  4:12 Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Usimjaribu Bwana Mungu wako."`

  4:13 Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.

  4:14 Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.

  4:15 Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.

  4:16 Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.

  4:17 Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:

  4:18 "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,

  4:19 na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana."

  4:20 Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.

  4:21 Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo."

  4:22 Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?"

  4:23 Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: `Mganga jiponye mwenyewe`, na pia mtasema: `Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."`

  4:24 Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.

  4:25 Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.

  4:26 Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.

  4:27 Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria."

  4:28 Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.

  4:29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.

  4:30 Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.

  4:31 Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.

  4:32 Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.

  4:33 Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:

  4:34 "We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!"

  4:35 Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.

  4:36 Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!"

  4:37 Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.

  4:38 Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.

  4:39 Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.

  4:40 Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.

  4:41 Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.

  4:42 Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.

  4:43 Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo."

  4:44 Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.

  IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

  God Rules.NET
  Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine