Bad Advertisement?

News / Reviews:
  • World News
  • Movie Reviews
  • Book Search

    Are you a Christian?

    Online Store:
  • Visit Our eBay Store



  • SWAHILI BIBLIA - MATTHEW 14

    JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


    14:1 Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu.

    14:2 Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."

    14:3 Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni

    14:4 kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!"

    14:5 Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.

    14:6 Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa,

    14:7 hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.

    14:8 Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji."

    14:9 Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe.

    14:10 Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.

    14:11 Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake.

    14:12 Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.

    14:13 Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini.

    14:14 Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao.

    14:15 Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula."

    14:16 Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula."

    14:17 Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili."

    14:18 Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa."

    14:19 Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.

    14:20 Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.

    14:21 Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.

    14:22 Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng`ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu.

    14:23 Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake,

    14:24 na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.

    14:25 Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji.

    14:26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu.

    14:27 Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"

    14:28 Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako."

    14:29 Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu.

    14:30 Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!"

    14:31 Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?"

    14:32 Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia.

    14:33 Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."

    14:34 Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti.

    14:35 Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote,

    14:36 wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.

    IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

    God Rules.NET
    Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine