Bad Advertisement?

News / Reviews:
 • World News
 • Movie Reviews
 • Book Search

  Are you a Christian?

  Online Store:
 • Visit Our eBay Store • SWAHILI BIBLIA - MATTHEW 25

  JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


  25:1 "Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.

  25:2 Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.

  25:3 Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.

  25:4 Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.

  25:5 Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.

  25:6 Usiku wa manane kukawa na kelele: `Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.`

  25:7 Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.

  25:8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: `Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.`

  25:9 Lakini wale wenye busara wakawaambia, `Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!`

  25:10 Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa.

  25:11 Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: `Bwana, bwana, tufungulie!`

  25:12 Lakini yeye akawajibu, `Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."`

  25:13 Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.

  25:14 "Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng`ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.

  25:15 Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.

  25:16 Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.

  25:17 Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.

  25:18 Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.

  25:19 "Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.

  25:20 Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, `Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.`

  25:21 Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`

  25:22 "Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, `Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.`

  25:23 Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`

  25:24 "Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, `Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya.

  25:25 Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.`

  25:26 "Bwana wake akamwambia, `Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.

  25:27 Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!

  25:28 Basi, mnyang`anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.

  25:29 Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

  25:30 Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.`

  25:31 "Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,

  25:32 na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.

  25:33 Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.

  25:34 "Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, `Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

  25:35 Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;

  25:36 nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.`

  25:37 Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme `Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?

  25:38 Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?

  25:39 Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?`

  25:40 Mfalme atawajibu, `Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.`

  25:41 "Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, `Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.

  25:42 Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.

  25:43 Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.`

  25:44 "Hapo nao watajibu, `Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?`

  25:45 Naye atawajibu, `Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.`

  25:46 Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele.

  IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

  God Rules.NET
  Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine