Bad Advertisement?

News / Reviews:
 • World News
 • Movie Reviews
 • Book Search

  Are you a Christian?

  Online Store:
 • Visit Our eBay Store • SWAHILI BIBLIA - MATTHEW 27

  JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


  27:1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.

  27:2 Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.

  27:3 Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha.

  27:4 Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako."

  27:5 Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.

  27:6 Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu."

  27:7 Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

  27:8 Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.

  27:9 Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei,

  27:10 wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza."

  27:11 Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema."

  27:12 Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.

  27:13 Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?"

  27:14 Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.

  27:15 Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.

  27:16 Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.

  27:17 Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba*fq* ama Yesu aitwae Kristo?"

  27:18 Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.

  27:19 Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake."

  27:20 Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

  27:21 Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!"

  27:22 Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!"

  27:23 Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!"

  27:24 Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe."

  27:25 Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!"

  27:26 Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe.

  27:27 Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.

  27:28 Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.

  27:29 Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!"

  27:30 Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.

  27:31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

  27:32 Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.

  27:33 Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa,"

  27:34 wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.

  27:35 Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.

  27:36 Wakaketi, wakawa wanamchunga.

  27:37 Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi."

  27:38 Wanyang`anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.

  27:39 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,

  27:40 "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!"

  27:41 Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,

  27:42 "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.

  27:43 Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka."

  27:44 Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.

  27:45 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza.

  27:46 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"

  27:47 Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya."

  27:48 Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.

  27:49 Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa."

  27:50 Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.

  27:51 Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

  27:52 makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;

  27:53 nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.

  27:54 Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu."

  27:55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.

  27:56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.

  27:57 Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.

  27:58 Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.

  27:59 Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani,

  27:60 akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.

  27:61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.

  27:62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,

  27:63 Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, `Baada ya siku tatu nitafufuka.`

  27:64 Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali."

  27:65 Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo."

  27:66 Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.

  IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

  God Rules.NET
  Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine