Bad Advertisement?

News / Reviews:
 • World News
 • Movie Reviews
 • Book Search

  Are you a Christian?

  Online Store:
 • Visit Our eBay Store • SWAHILI BIBLIA - REVELATION 18

  JANA SURA - IJAYO SURA - AMARA


  18:1 Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng`ao wake.

  18:2 Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, "Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno.

  18:3 Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo."

  18:4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, "Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake.

  18:5 Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake.

  18:6 Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni.

  18:7 Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: `Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!`

  18:8 Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo."

  18:9 Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea.

  18:10 Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, "Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata."

  18:11 Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao;

  18:12 hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari;

  18:13 mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng`ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu.

  18:14 Wafanyabiashara wanamwambia: "Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!"

  18:15 Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza,

  18:16 wakisema, "Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu!

  18:17 Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!" Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali,

  18:18 na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: "Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!"

  18:19 Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: "Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!"

  18:20 Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi!

  18:21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, "Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa.

  18:22 Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako.

  18:23 Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!"

  18:24 Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani.

  IJAYO SURA - BIBLIA MWELEZO & UTAFUTAJI

  God Rules.NET
  Search 100+ volumes of books at one time. Swahili Biblia Search Engine. Hausa Biblia Search Engine. Afrikaan Bible Search Engine